Kristendommen// Ukristo
Ukristo ulianzishwa takribani miaka 2,000 iliyopita katika Mashariki ya Kati, katika eneo ambalo sasa ni Israeli na Palestina. Wakati huo, watu wengi katika Mashariki ya Kati walikuwa Wayahudi. Neno Ukristo linatokana na Yesu Kristo.
Ukristo ndio dini kubwa zaidi duniani. Watu wanaoamini katika dini ya Ukristo wanaitwa Wakristo. Kuna takriban ya wakristo bilioni 2.3 duniani. Katika kufanana na wayahudi na waislamu, wakristo wanaamini kwamba kuna Mungu mmoja tu. Kwa hivyo, dini hizo tatu zinaitwa dini za kuamini katika Mungu alie mmoja tu.
Baada ya kuanzishwa kwa Ukristo, dini ilikendelea kukua katika njia tofauti. Ni kawaida kugawanya Ukristo katika pande kuu tatu. Pande hizi ni Kanisa Katoliki, Kanisa la Orthodox na Kanisa la Kiprotestanti. Jambo la pamoja kwa pande zote ni kwamba wanaona Biblia ni kitabu kitakatifu na kwamba Yesu Kristo ni mwana wa Mungu.
Imani
Wakristo wanaamini katika Mungu mmoja aliyepo katika maumbo matatu. Maumbo hayo ni Mungu Baba, Mwana (Yesu Kristo), na Roho Mtakatifu. Hii inaitwa Utatu mtakatifu wa Mungu.
Kulingana na Biblia, Mungu aliumba ulimwengu, na Yesu alikuwa mwana wake (mtoto wa Mungu). Yesu ndiye nabii muhimu zaidi wa Ukristo. Alipaswa kuwafundisha watu kuhusu Mungu ili kuwapa tumaini. Biblia inasema kwamba Yesu alikufa msalabani na kufufuka kutoka katika wafu. Roho Mtakatifu hutoa mwongozo, nguvu, na faraja kwa wale wanaoamini.

Imani ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku kwa Wakristo wengi. Wakristo wanaweza kusali kila siku na kusoma Biblia. Wanaweza kushiriki katika ibada za kanisa na shughuli zingine za kanisa. Maadili muhimu katika Ukristo ni upendo, msamaha, na huruma. Wakristo wanahimizwa kujitolea na kuwasaidia wale wenye uhitaji
Watu watakatifu
Katika Ukristo, kuna watu wengi wanaochukuliwa kuwa watakatifu au wana umuhimu maalumu. Wanaonekana kama mifano ya kuigwa kwa sababu ya ukaribu wao na Mungu.
Mtu muhimu zaidi katika Ukristo ni Yesu. Mama yake anaitwa Bikira Maria. Yeye ni mfano wa imani, utii, na unyenyekevu. Yesu alikuwa na mitume 12 ambao walikuwa wanafunzi wake. Baada ya Yesu kufa, wanafunzi walipewa jukumu la kueneza (injili) ujumbe wake kwa watu. Walipaswa kuelezea yale ambayo Yesu alisema na kufanya alipokuwa akiishi duniani.
Katika mila na desturi za Wakatoliki na Waorthodoksi, watakatifu huchukuliwa kuwa ni watu ambao wameishi maisha matakatifu na ya mfano. Mtakatifu Lucia ni mfano mmoja wa mtakatifu. Tarehe 13 mwezi wa kumi na mbili (desemba) huadhimishwa kama kumbukumbu ya Siku ya Lucia.

Vitabu vitakatifu
Biblia ni kitabu kitakatifu katika Ukristo. Kina Agano la Kale na Agano Jipya. Agano la Kale lina maandishi kuhusu watu muhimu na matukio ya tangu wakati Yesu hajazaliwa. Vitabu vya Mwanzo ni sehemu ya Agano la Kale. Vinajumuisha hadithi za Ibrahimu na Musa. Maandiko haya pia ni muhimu kwa Uislamu na Uyahudi.
Agano Jipya lina maandiko kuhusu maisha ya Yesu na jinsi ujumbe wake ulivyosambazwa. Agano Jipya ni muhimu kwa imani na matendo ya Kikristo.

Nyumba ya Mungu
Nyumba za Mungu za wakristo huitwa makanisa. Kanisa ndilo mahali muhimu zaidi pa kukusanyika kwa shughuli za kidini na kijamii. Huko, Wakristo hukutana kwa ajili ya maombi, masomo, na ibada ya pamoja. Kanisa pia hutumika kwa ajili ya kufundisha, kusherehekea sikukuu, na shughuli zingine zinazojenga jamii. Ibada huongozwa na Mchungaji, kuhani, padri au kasisi anayesimulia na kusoma hadithi kutoka kwenye Biblia. Wale wanaoshiriki katika ibada huitwa waumini.
Makanisa yanaweza kutofautiana kwa ukubwa na muundo. Kama ishara ya Ukristo, makanisa mengi yana angalau mnara wa kengele na msalaba. Kengele za kanisa hulia kutangaza kwamba kuna ibada au sherehe nyingine kanisani.





Sikukuu na ibada ya sala za matambiko
Baadhi ya sikukuu muhimu zaidi katika Ukristo ni Krismasi, Pasaka, na Pentekoste. Sikukuu hizo huadhimisha matukio muhimu katika historia ya dini hiyo.
Sikuuu ya Krismasi tunasherekea na kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu. Wakristo wengi husherehekea kwa ibada za kanisa, zawadi, na sherehe za kifamilia. Pasaka huadhimisha kifo cha Yesu msalabani na kufufuka kwake kutoka kaburini. Pentekoste huadhimisha ujio wa Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wa Yesu (mitume wa Yesu), akiwapa uwezo wa kuzungumza au kunena na kuelewa lugha zote. Pentekoste inachukuliwa kuwa mwanzo wa kanisa la Kikristo.
Matawi tofauti ya Ukristo yanaweza kuwa na mila au desturi za sala za matambiko tofauti. Kile ambacho mila hizo zinafanana ni kwamba zinakusudiwa kuwasaidia waumini kupata uzoefu na ukaribu na Mungu, umoja na ushirika katika kutaniko la kanisa. Mifano ya mila za Kikristo ni ubatizo, ushirika wa ekaristi na kipaimara.


