Landsdeler og fylker i Norge // Sehemu katika Nchi ya Norway na Mikoa.
Norway ina sehemu gani za nchi? Je, nchi imegawanywa katika mikoa mingapi?
Mkoa wa Finnmark, Mkoa wa Telemark, Mkoa wa Rogaland, Mkoa wa Troms, Mkoa wa Buskerud, Mkoa wa Vestland, Mkoa wa Nordland, Mkoa wa Akershus, Mkoa wa Møre na Romsdal, Oslo, Mkoa wa Østfold, Mkoa wa vestfold na Mkoa wa Innland
Ni kawaida kugawanya Norway katika sehemu tano za katika Nchi: Kaskazini mwa Norway, Trøndelag, Mashariki mwa Norway, Kusini mwa Norway na Magharibi mwa Norway. Kila sehemu ya nchi kuna mkoa au kaunti moja au zaidi (mikoa mingi) .
Kuna mikoa au kaunti 15 nchini Norway. Mikoa au kaunti hizo ni sehemu ya utawala, inamaanisha kwamba inatawaliwa kisiasa. Ni mabaraza ya mikoa au kaunti yanayosimamia mikoa au kaunti. Wajumbe wa mabaraza ya kata huchaguliwa na wananchi.
Norway ya Kaskazini
Kaskazini mwa Norway iko kaskazini zaidi mwa nchi. Sehemu hii ya nchi ina mikoa au kaunti tatu ya Finnmark, Troms na Nordland.
Sehemu kubwa zaidi ya Kaskazini mwa Norway iko kaskazini mwa Mzingo wa Aktiki. Kaskazini mwa Mzingo wa Aktiki, kuna giza kwa sehemu ya majira ya baridi kali na jua la usiku wa manane kwa sehemu ya kiangazi. Wakati wa giza, mtu huwezi kuona jua wakati wote wa mchana. Katika kipindi cha jua la usiku wa manane, unaweza kuona jua wakati wa mchana na usiku. Kadiri unavyoenda kaskazini, ndivyo siku zinavyozidi kuwa zaidi na jua la usiku wa manane na giza kwa kipindi chote cha baridi. Kwenye Rasi ya Kaskazini (Nordkapp), ni giza kuanzia tarehe 20 mwezi wa kumi na moja hadi tarehe 22 mwezi wa kwanza, na jua la usiku wa manane kuanzia tarehe 14 mwezi wa tano au mei hadi tarehe 29 mwezi wa saba.
Katika kaskazini mwa Norway, unaweza kuona mwangaza (taa) za kaskazini wakati wa baridi. Mwangaza (taa) za kaskazini ni taa za kijani kibichi na za waridi zinazotikisika au kutembea angani.
Mkoa wa Finnmark
Finnmark iko sehemu ya mbali zaidi ya kaskazini na mbali zaidi ya mashariki ya Norway na inapakana na nchi ya Urusi na Finland au Ufini. Finnmark ni mkoa au kaunti ya pili kwa ukubwa nchini Norway katika eneo hilo na ndogo zaidi kwa idadi ya watu. Nordkapp (Rasi ya kaskazini) ni kivutio maarufu cha watalii huko Finnmark. Nordkapp (Rasi ya kaskazini) mara nyingi hujulikana kama sehemu ya kaskazini mwa Norway na Ulaya. Hii sio sahihi kabisa, kwa sababu Knivskjellodden ipo karibia au takribani kilomita 1.5 zaidi kuelekea kaskazini.
Wasami wengi wanaishi Finnmark, na lugha ya Kisami iko na nafasi sawa na lugha ya Kinorway katika maeneo mengi katika mkoa. Bunge la wasami ni chombo kilichochaguliwa ambacho jukumu lake au kazi yake ni kuhakikisha na kusimamia haki, lugha na utamaduni wa Wasami. Bunge la Sami liko Karasjok.
Mkoa wa Troms
Troms ni mkoa wa pili kutoka kaskazini mwa Norway. Mkoa una mpaka na nchi ya Finland au Ufini. Tromsø ni jiji kubwa zaidi la mkoa au kaunti, na pia jiji kubwa zaidi kaskazini mwa Norway. Kanisa maarufu huko Tromsø ni Kanisa kuu la Arctic. Umbo la jengo linaweza kufanana na barafu isiyoyeyuka na milima.
Mkoa wa Nordland
Nordland ni mkoa mrefu na mwembamba unaopakana na nchi ya Swideni au Uswidi. Bodø ni mji mkubwa zaidi ndani ya Nordland.
Lofoten iko ndani ya Nordland na ina visiwa vingi. Kuanzia mwezi wa kwanza hadi mwezi wa nne, idadi kubwa ya samaki aina ya skrei huvuliwa huko Lofoten. Skrei ni samaki chewa wanaoishi mbali kaskazini katika Bahari ya Barents kwa muda mrefu ndani ya mwaka. Samaki Skreiene wanakuja pwani kuweka mayai katika kipindi cha mwezi wa kwanza hadi mwezi wa nne. Samaki wengi wa skrei wanakaushwa. Samaki wakavu huitwa samaki waliokaushwa kwa kinorway tørrfisk. Wengi wa samaki waliokaushwa husafirishwa kwenda nchi nyingine, kama vile Italia na Nigeria.
Kule Kaskazini mwa mzingo wa Aktiki unapitia Nordland. Kaskazini mwa mzingo wa Aktiki kuna giza na jua la usiku wa manane.
Trøndelag
Trøndelag iko katikati ya nchi na ni sehemu ya nchi na mkoa. Sehemu ya nchi hii pia inaitwa Norway ya kati kwa kinorway Midt-Norge. Trøndelag ina fiodi ndefu, maeneo ya kilimo yenye rutuba na milima mirefu. Fiodi ndefu zaidi katika Trøndelag ni Trondheimsfjorden na Trollhetta ndio mlima mrefu zaidi. Trøndelag ina mpaka na Swideni au Uswidi.
Mji mkubwa zaidi katika Trøndelag ni Trondheim. Trondheim ni mji wa tatu kwa ukubwa nchini Norway. Nidarosdomen ni kanisa kuu maarufu huko Trondheim. Nidarosdomen ni kanisa kuu la kaskazini zaidi la zama za kati za kanisa duniani.
Røros ni mji unaopatikana katika mkoa wa Trøndelag. Røros iko juu katika milima ya Røros. Mji huo ulianzishwa au ulitengenezwa kwa sababu walipata madini ya shaba katika milima hiyo mnamo mwaka wa 1644. Migodi ya madini ya shaba ilitengenezwa. Watu walihamia Røros kufanya kazi katika migodi. Hivi ndivyo mji wa Røros ulivyokua.
Norway ya mashariki
Norway ya Mashariki au sehemu ya mashariki ya nchi iko katika sehemu ya kusini-mashariki ya nchi. Norway ya Mashariki au sehemu ya mashariki ya nchi kwa kinorway Østlandet ina mikoa au kaunti 6. kuna Oslo, Vestfold, Telemark, Buskerud, Akershus na Innlandet. Norway ya Mashariki au Østlandet ina mandhari mbalimbali yenye maeneo tambarare ya kilimo katika mashariki na maeneo ya milimani upande wa magharibi. Eneo pia lina maziwa kadhaa makubwa, kama vile Mjøsa na Tyrifiodi au kwa kinorway Tyrifjorden. Østlandet ndiyo sehemu kubwa na yenye watu wengi zaidi nchini Norway. Takribani nusu ya wakazi wa Norway wanaishi Mashariki mwa nchi ya Norway (Østlandet).
Mjøsa
Oslo
Oslo ni mji mkuu wa Norway na jiji kubwa zaidi nchini Norway. Mji uko ndani kabisa ya Oslofiodi. Alama zinazojulikana sana huko Oslo ni Jumba la Kifalme, Bunge, Jengo la Opera na bustani ya Frogner. Bustani ya Frogner ni bustani inayojulikana kwa sanamu zake nyingi.
Mkoa wa Vestfold
Vestfold iko magharibi mwa Oslofiodi au kwa kinorway Oslofjord na ndiyo mkoa mdogo zaidi kwa eneo. Mkoa huo una ukanda wa pwani mrefu na Mkusanyiko wa visiwa vingi kwa pamoja, visiwa vingi vidogo na miamba. Tønsberg ni mji mkubwa zaidi katika Vestfold na pia inachukuliwa kuwa ni mji mkongwe au wa zamani zaidi wa Norway.
Huko Vestfold, uvumbuzi mwingi wa kiakiolojia umefanywa kutoka enzi ya zama za Viking, pamoja na meli ya Oseberg. Meli ya Oseberg ilipatikana katika kilima kikubwa cha kuzikia huko Tønsberg. Meli hiyo ilitumika kama meli ya mazishi kwa wanawake wawili.
Mkoa wa Telemark
Telemark inaenea kwa kuongezeka kutoka pwani hadi kwenye milima mirefu. Skien na Porsgrunn ndio miji mikubwa zaidi katika mkoa.
Mji wa Rjukan, ambao uko kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia wa UNESCO, uko ndani ya Telemark. Mji huu ulianzishwa mwanzoni mwa karne ya 19 na Norsk Hydro kwa kuzalisha mbolea bandia ili kuongeza usalama wa uzalishaji wa chakula ndani ya Norway na Ulaya.
Gaustatoppen ni mlima mrefu zaidi uliopo Telemark. Moja ya vivutio huko Gaustatoppen ni Gaustabanen. Gaustabanen ni gari la kamba ya umeme au kebo ambalo hupita kwenye njia ya reli iliyochimbwa chini ya ardhi/mlima (handaki), njia inaanzia chini ya mlima hadi juu.
Mkoa wa Buskerud
Buskerud iko magharibi mwa Oslofiodi na inaeneo kutoka pwani hadi juu ya Hardangervidda. Hardangervidda ni takriban kilomita za mraba 8,000 na ni uwanda wa juu zaidi wa milima mirefu Kaskazini ya ulaya. Uwanda wa juu wa mlima ni eneo kubwa na tambarare ambalo liko juu ya usawa wa bahari. Uwanda wa juu wa mlima au kwa kinorway Høyfjellsplatå wakati mwingine pia huitwa vidde ambalo ni eneo tambarare juu ya mlima.
Miji mikubwa zaidi katika Buskerud ni Drammen, Kongsberg na Hønefoss. Drammen iko pembeni ya mto Drammen (Drammenselva), ambayo ni kati ya mito mikubwa nchini Norway. Kongsberg inajulikana zaidi kwa migodi yake ya madini ya fedha. Migodi ya madini ya fedha haifanyi kazi tena lakini imebadilishwa kuwa majumba ya makumbusho.
Mkoa wa Akershus
Mkoa wa Akershus ni mkoa mdogo wa tatu kwa eneo, lakini kwa idadi ya watu ni mkoa wa pili kwa ukubwa, una takribani wakazi 700,000. Mkoa huo unaanzia kusini mwa Oslofiodi hadi Mjøsa kwa kaskazini . Akershus ina mazingira tofauti tofauti kama pwani, mazingira ya kilimo na misitu.
Eidsvoll iko kaskazini mwa mkoa wa Akershus, kusini mwa Mjøsa. Eidsvoll inajulikana kwa jengo la Eidsvoll. Ilikuwa katika jengo hili ambapo katiba ya Norway iliandikwa mnamo mwaka 1814.
Uwanja wa ndege mkuu wa Norway uko Gardermoen, ambao uko takribani katikati mwa mkoa wa Akershus.
Mkoa wa Østfold
Østfold ndiyo mkoa wa mbali zaidi kusini-mashariki nchini. Mkoa huu una mpaka na Swideni au Uswidi. Miji mikubwa zaidi katika mkoa huu ni Fredrikstad na Sarpsborg. Mto mrefu zaidi nchini Norway, Glomma, unatiririka kupitia Sarpsborg na kuishia Fredrikstad.
Fredrikstad na Halden ni miji inayojulikana sana huko Østfold. Mji Mkongwe huko Fredrikstad unachukuliwa kama mji wenye ngome Kaskazini mwa Ulaya uliohifadhiwa vyema. Ngome zenyewe zilianzia karne ya 16 au miaka ya 1600.
Ngome ya Fredriksten ni ngome ya kihistoria iliyoko Halden. Ngome hiyo ilijengwa mnamo mwaka 1661 kama jengo la kujihami au la kazi za ulinzi pembeni ya mpaka na Swideni au Uswidi. Leo, Ngome ya Fredriksten ni kivutio maarufu kwa watalii.
Mkoa wa Innlandet
Mkoa wa Innlandet ni mkoa mkubwa zaidi kwa eneo na ni mkoa pekee ambao hauna ukanda wa pwani. Innlandet inaanzia kwenye maeneo yenye rutuba ya kilimo mashariki hadi kwenye milima mirefu magharibi. Mkoa huu unapakana na Swiden au Uswidi. Miji mikubwa zaidi ni Hamar, Lillehammer na Gjøvik. Miji hii yote iko karibu na ziwa Mjøsa, ambalo ni ziwa kubwa zaidi la Norway.
Maeneo mawili ya milimani yanayojulikana sana nchini Norway ni Dovrefjell na Jotunheimen. Yote mawili yako Innlandet. Milima miwili mirefu zaidi nchini Norway, Galdhøpiggen na Glittertind, iko Jotunheimen.
Innlandet ndiyo mkoa mkubwa zaidi wenye nyumba ndogo kwa kinorway hytte (nyumba za likizo/mapumziko au vibanda), ina takribani nyumba ndogo 90,000 au nyumba za likizo au mapumziko. Nyumba ndogo nyingi ziko karibu na maeneo ya watalii yanayojulikana, kwa mfano Trysil, Hafjell na Kvitfjell, ambayo zote ni sehemu zinazojulikana za kwenda kwa kutereza kwenye barafu (skiing), wakati wa baridi na kwa shughuli nyingine za nje katika majira ya kiangazi au joto.
Mkoa wa Sørlandet
Kuna Mkoa mmoja tu Kusini mwa Norway au sørlandet, ambao ni Agder. Kusini mwa Norway au sørlandet ina visiwa vizuri vidogo na visiwa vikubwa, na maeneo mengi ya kuoga au kuogelea. Kusini mwa Norway au sørlandet ni sehemu inayovutia na maarufu kwa likizo za majira ya joto, fukwe nyingi, maeneo ya kuweka kambi na nyumba za likizo kando ya pwani.
Kusini mwa Norway (Sørlandet) kunajulikana kwa miji yake midogo yenye mitaa miyembamba na nyumba za mbao zilizopakwa rangi nyeupe, kwa mfano Risør na Grimstad, ambazo mara nyingi huhusishwa na nyumba zao za mbao zilizopakwa rangi nyeupe. Miji miwili mikubwa ya Kusini mwa Norway (Sørlandet) ni Kristiansand na Arendal.
Sehemu iliyo kusini zaidi mwa Norway ni Lindesnes. Mnara wa taa wa Lindesnes ulijengwa mnamo mwaka 1656 na ndio mnara wa zamani zaidi nchini Norway. Bado unafanya kazi na kuna jumba la kumbukumbu lililounganishwa na mnara wa taa.
Magharibi mwa Norway
Magharibi mwa Norway au kwa kinorway Vestlandet ina mikoa mitatu ya Møre na Romsdal, Vestland na Rogaland. Uasilia katika Magharibi ya Norway (Vestlandet) ina sifa ya fiodi ndefu na zenye kina kirefu na ardhi ya mwinuko yenye milima mirefu. Fiodi ndefu (sehemu ya bahari iliyo ingia ndani ya nchi kavu ) zaidi Norway, Sognefjord iko Magharibi mwa Norway au Vestlandet. ina urefu wa kilomita 204. Miji mikubwa zaidi katika eneo hilo ni Bergen, Stavanger, Ålesund na Haugesund. Magharibi mwa Norway au Vestlandet inajulikana kwa vyakula vyake vya baharini, haswa samaki aina ya laks na samaki klipp kwa kinorway, na kwa sekta ya viwanda vyake vya mafuta.
Mkoa wa Rogaland
Mji mkubwa zaidi huko Rogaland ni Stavanger. Mafuta yalipatikana katika Bahari ya Kaskazini au Nordsjøen mwishoni mwa miaka ya 1960. Iliamuliwa kuwa makao makuu ya sekta ya viwanda vya mafuta viwepo Stavanger. Kulikuwa na wafanyakazi wanne hapo mwanzoni. Mmoja wao alitoka Iraq na anaitwa Farouk Al-Kasim.
Mkoa wa Vestland
Mji mkubwa zaidi katika Vestland ni Bergen. Bergen ni jiji la pili kwa ukubwa nchini Norway, na jiji hilo mara nyingi huitwa mji mkuu wa Magharibi mwa Norway (Vestland). Bryggen ndani ya Bergen ni sehemu inayojulikana sana huko Bergen.
Kuna barafu isiyoyeyuka nyingi nchini Norway. Barafu isiyoyeyuka ni eneo kubwa linalokuwa na barafu. Katika baadhi ya maeneo ni baridi sana katika majira ya kiangazi au joto na kwamba barafu au theluji haiwezi kuyeyuka. Hivyo kunakuwa na barafu au theluji zaidi na zaidi kila mwaka. Barafu au theluji inayodondoka hatimaye inaganda au inageuka na kuwa barafu. Wakati eneo la barafu linakuwa kubwa na zito kiasi kwamba huanza kuteleza chini ya mlima, hiyo huitwa barafu isiyoyeyuka kwa kinorway Isbre. Jostedalsbreen ndio barafu kubwa zaidi nchini Norway isiyoyeyuka. Jostedalsbreen iko katika sehemu ya mkoa au kaunti ya Vestland.
Mkoa wa Møre na Romsdal
Mji mkubwa zaidi katika mkoa wa Møre na Romsdal ni Ålesund. Kulikuwa na moto mkubwa huko Ålesund mwaka 1904. Karibu sehemu yote ya mjini Ålesund iliteketea kwa moto. Mji ulijengwa upya kwa mtindo wa Art Nouveau. Ilikuwa ni wasanifu majengo wa Ujerumani ambao walipanga usanifu mpya.
Maporomoko ya maji ya juu kabisa ya Norway yanapatikana Møre og Romsdal, yanaitwa maporomoko ya maji ya Vinnu au vinnufossen. Hakuna maji mengi katika maporomoko ya maji ya juu zaidi nchini Norway. Ngazi ya Midsund ni ngazi za mawe zenye hatua 2,200. Zilijengwa na Sherpas kutoka Nepal.
Picha ambazo hazijatambulishwa kwa kuwekewa alama zimepewa leseni kutoka kwa AdobeStock
Jifunze zaidi kuhusu Norway katika Samfunnskunnskap.no
Katika Samfunnskunnskap.no kuna filamu, maandishi na kazi shirikishi kuhusu Norwei katika lugha nyingi au kadhaa.
Dette er Norge: Fakta om Norge (samfunnskunnskap.no)
Hii ni Norwei: Ukweli kuhusu Norway (samfunkskunnskap.no)