Hva er demokrati?// Demokrasia ni nini?

Denne teksten finnes på flere språk. Teksten er en litt bearbeidet versjon av fagteksten med samme tittel på NDLA.no. NDLA er forkortelse for Nasjonal digital læringsarena. NDLA produserer gratis læringsressurser for videregående opplæring. Oversettelsene til ulike språk kan brukes i innledning til arbeid med temaet. Teksten kan også brukes sammen med tospråklig lærer for å aktivere elevenes kunnskaper om temaet, og til å bidra til at eleven lærer fagspråk.

Kilde: Zakariassen, E. S. (2024, 5. mars). Hva er demokrati?. NDLA. https://ndla.no/r/samfunnskunnskap/hva-er-demokrati/d3692431fa


Demokrasia ina maanisha ni uongozi wa watu (watu ndio wanao ongoza). Lakini ina maana gani tunaposema kuwa nchi ina demokrasia? Je inatosha kwa sababu kila mtu ana haki ya kupiga kura (kuamua) au ni kuhusu jambo lingine zaidi?

Fotografi av en hånd som holder en stemmeseddel delvis inne i sen orange stemmeurne
Haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa kisiasa ni moja ya haki za msingi katika demokrasia

Aina tofauti za demokrasia

Nchi nyingi duniani zinajiita kuwa ni nchi za kidemokrasia. Nchi nyingi kati ya hizo zina demokrasia inayofanya kazi vibaya. Muda fulani tunaweza ziita kuwa zina muonekano tu wa nje wa kidemokrasia. Hizi ni nchi zinazojaribu kuonyesha kuwa ni za kidemokrasia. Kwa mfano kwa kufanya uchaguzi, lakini usioweza kuitwa uchaguzi wa haki na kidemokrasia kwa sababu kunakuwa na udanganyifu kwenye uchaguzi, kukosekana kwa haki za kisiasa ama kuna kuwa na mtu mwingine ambaye hajachaguliwa na watu ambae anaongoza nchi.

Kuna njia mbili kuu za kupangilia demokrasia. Demokrasia ya moja kwa moja na ile isiyo ya moja kwa moja (pia inaitwa demokrasia ya kuwakilishwa)

Demokrasia ya moja kwa moja

Demokrasia ya moja kwa moja ni demokrasia ambayo maswali ya kisiasa yanaamuliwa na wananchi wenyewe wanamaua moja kwa moja kwa kutumia kura ya maoni (kura ya maoni ni kura ambayo watu wanapiga kura kutoa maoni au kuamua juu ya jambo fulani). Hakuna nchi siku hizi yenye demokrasia ya moja kwa moja, lakini nchi nyingine wanatumia mara nyingi kura ya maoni (kura ambayo watu wanapiga kura kutoa maoni au kuamua juu ya jambo fulani) zaidi ya nchi nyingine. Norwe mara ya mwisho kutumia kura ya maoni kwa taifa lote ilikuwa mwaka 1994, ambapo wa Norwe waliamua hawataki kuwa wanachama wa umoja wa ulaya (EU).

Demokrasia isiyokuwa ya moja kwa moja

Demokrasia isiyokuwa ya moja kwa moja au demokrasia ya uwakilishi ni demokrasia ambayo watu wanachagua wawakilishi katika kuongoza nchi kwa ajili yao wote. Demokrasia zote hasa za kisasa au siku hizi zinaongozwa kwa njia hii.

Foto av en blå skive med teksten EU. til høyre står det Ja, og til venstre står det nei. Den røde pila står på nei-siden
Kutoka kura ya maoni au ya mapendekezo ndani ya Norwe mwaka 1994. Hii ilikuwa mara ya mwisho Norwe ilitumia demokrasia ya moja kwa moja katika ngazi ya taifa. Je unajua kura ya maoni nyingine iliyowahi kutumika ?

Ni nini kinachofanya nchi kuwa ya kidemokrasia?

Neno demokrasi limetokana na maneno ya Kigiriki demos (watu) na kratos (utawala), na linamaanisha utawala wa watu. Wazo kwamba watu wote wanaweza kuathiri namna jamii inatawaliwa, inajengwa juu ya fikra au mawazo kwamba binadamu wote wana thamani sawa, kama vile inavyoelezwa katika kifungu cha kwanza cha tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Watu wote wamezaliwa huru, wakiwa na thamani sawa na haki sawa za kibinadamu. Wote wamejaliwa akili na dhamiri, hivyo inapaswa kutendeana kwa roho ya kindugu (Azimio la Haki za Binadamu la Ulimwengu la mwaka 1948, Kifungu cha 1)

Hapa tutazungumzia kabla ya yote demokrasia kama namna ya utawala katika nchi. Tunaweza pia kupata demokrasia, au kitu kinachofanana nacho, katika vilabu vya michezo, makampuni, shuleni, katika familia na kati ya marafiki.

Watu wengi wanaweza kufikiria kwamba neno demokrasia linahusiana na nchi zenye uchaguzi wa kisiasa ambamo watu wazima wote wana haki ya kupiga kura. Lakini ina maana gani kusema kwamba watu ndiyo wanaotawala katika nchi? Ili kuelewa hilo, tutatazama kwa karibu kanuni tatu muhimu ambazo lazima ziwepo ili nchi iweze kujiita ni ya kidemokrasia. Kanuni hizo ni:

  1. Haki sawa za kidemokrasia
  2. Fursa sawa za kidemokrasia
  3. Kulinda maslahi ya mtu mmoja mmoja na ya makundi madogo (watu waliowachache)

Haki sawa za kidemokrasia

Kitu cha msingi zaidi kama nchi inasema kuwa ni ya kidemokrasia, ni watu wote kuwa na haki sawa za kidemokrasia. “Wote” inamaanisha watu wazima wote ambao ni raia katika nchi. Haki sawa za kidemokrasia zinahakikishwa kupitia haki ya kupiga kura, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika pamoja katika vyama na watu wengine.

Haki ya kupiga kura

Haki ya kupiga kura ni haki ya kisiasa katika demokrasia. Kwa mfano Norwe raia wote wa Norwei wenye miaka kuanzia 18 au waliofikisha miaka 18 na zaidi wana haki ya kuchagua mtu katika uchaguzi wa wabunge. Kuna mifano mingi ya makundi mbalimbali katika jamii ambayo hayaja kuwa na haki ya kupiga kura. Kwa mfano, wanawake, maskini, na makabila madogo walitengwa katika upigaji kura katika nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Norwe. Katika baadhi ya nchi nyingine, hali hii bado ipo. Vizuizi kama hivyo vya haki za kupiga kura hufanya nchi kuwa na demokrasia kidogo.

Ili haki ya kupiga kura iwe na maana yoyote, ni muhimu uchaguzi uandaliwe kwa njia ambayo inayochukuliwa kuwa ni ya kidemokrasia na ya haki. Isitoshe, lazima kuwe na mipango inayozuia udanganyifu wa kuiba kura na ulaghai wa udanganyifu wa makusudi, hivyo inaitwa udanganyifu katika uchaguzi. Matokeo ya uchaguzi lazima pia yawe na umuhimu kwa siasa zinazoendeshwa nchini. Hii ina maana kwamba viongozi waliochaguliwa lazima wawe na mamlaka ya kuongoza. Haifai kuwa na uchaguzi za kisiasa ikiwa mtu mwingine mbali na viongozi waliochaguliwa anakuwa kiongozi wa nchi.

foto av en kvinnehånd som holder fram pekefinger som er merket med blekk
Katika nchi nyingi huweka alama ya wino kwenye kidole kuzuia mtu asipige kura mara nyingi. Hapa mwanamke mmoja anaonesha kuwa ameshapiga kura. Je ni kwa nini haitoshi kusema kuwa nchi ni ya kidemokrasia kwa kuwa watu wanapiga kura katika uchaguzi?

Uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika pamoja katika chama na kuwa na watu wengine.

Kuchangia na kushiriki kisiasa ni zaidi ya kuwa na haki ya kupiga kura. Kwa kuongezea kila mtu kwenye demokrasia ana haki ya kushiriki kwenye siasa. Haijalishi miaka ya mtu aliyonao. Tunaweza andika kwenye gazeti, kwenda kwenye maandamano, kuanzisha kampeni ya kukusanya saini ama kujiunga katika chama cha wafanyakazi ama chama cha siasa ama kushiriki katika uchaguzi kama mwanasiasa. Ili kuhakikisha kuwa tuna uhuru wa kukusanyika pamoja na watu wengine kwenye chama na kuwa na uhuru wa kujieleza.

Fursa sawa katika demokrasia

Demokrasia inayofanya kazi lazima iwe na malengo ya kuwa na watu wengi zaidi wanao shiriki katika demokrasia. Unapopiga kura katika uchaguzi, unatoa ruhusa kwa yule unayempigia kura kwa kipindi fulani. Kwa Norwe kipindi cha uongozi ni cha miaka minne. Hii ina maanisha wale watakao chaguliwa, wanapata nguvu zaidi ya kufanya maamuzi zaidi ya wengine, lakini ili kuzuia waliochaguliwa wasitumie nguvu ya kufanya ya uongozi vibaya wanayopata, inabidi kuiwekea mipaka au kikomo.

Ili kuhakikisha fursa za kutosha na sawa za kidemokrasia inabidi tuwe na watu wengi wanao weza kushiriki katika demokrasia, na wakati huo huo kuwekea mipaka ya nguvu ya uongozi kwa watu waliochaguliwa. Kuna njia mbali mbali za kufanya hili. Tutaenda kuona baadhi ya njia hizo:

Kuongeza ushiriki wa watu katika uchaguzi.

Ingawa watu wote wana haki sawa ya kushiriki na kuchangingia katika siasa, haimaanishi kuwa watu wote wanatumia haki hiyo. Kwanza watu wanaweza kuacha kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi. Katika uchaguzi wa bunge Norwe mwaka 2021 kulikuwa na 20% ya watu ambao wangeweza kupiga kura, ambao hawakupiga kura. Kiuhalisia ni ngumu kuweza kufanya watu wote wakapiga kura, lakini ni malengo ya kidemokrasia Norwe kuwa watu wengi kwa jinsi inavyowezekana waweze kupiga kura wakati wa uchaguzi.

Ujuzi na upatikanaji wa habari

Ili watu waweze kuelewa mfumo wa kisiasa na kuweza fuatilia yanayoendelea, ni lazima wawe na ujuzi na kuwe na upatikanaji wa habari. Katika baadhi ya nchi, ni vigumu kufikia demokrasia kutokana na idadi (viwango) kubwa vya watu kutokuwa na uwezo wa kusoma na kuandika. Kwa hiyo, haki ya kupata elimu ni ya muhimu kwa demokrasia kuweza kufanya kazi.

Bilde av elever som slitter i klassen. Noen av dem rekker opp hånda.
Mfumo mzuri wa shule ni muhimu kwa kuwezesha kuwa na demokrasia. Je, unaweza fikiria kwamba sasa hivi ukiwa umekaa na kusoma kuhusu demokrasia, kwa uhalisia ni sehemu muhimu ya kidemokrasia?

Mbali na kwenda shule, lazima pia mtu awe na uwezo wa kufuatilia siasa zinazoendeshwa katika nchi. Demokrasia inahitaji vyombo huru vya habari na visivyoegemea upande wowote vinavyoweza kuripoti juu ya kile kinachotokea, kutoa maoni tofauti na kufichua hali mbaya katika jamii bila kukaguliwa. Wakati kila mtu ana nafasi ya kwenda shule na vyombo vya habari, kila mtu pia ana nafasi ya kushiriki katika kidemokrasia.

Mgawanyo wa madaraka

Wawakilishi wa wananchi katika bunge au wabunge na viongozi wa kwenye serikali wana nguvu zaidi kisiasa kuliko watu walio wengi katika nchi. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa katika demokrasia ya uwakilishi ambapo tunamchagua mtu wa kutawala nchi badala ya sisi wote kuwa tunaongoza nchi. Lakini kuna njia kadhaa za kupunguza nguvu hii ili tuepuke matumizi mabaya ya uongozi (madaraka). Demokrasia nyingi hufuata kile kinachoitwa kanuni ya mgawanyo wa uongozi (madaraka). Hii ina maana kwamba kazi muhimu zaidi za serikali zimegawanywa katika ofisi za kiserikali (taasisi) tatu tofauti.

Aina ya madaraka

Kazi

Taasisi

Bunge au Mamlaka ya kutunga sheria

Inatengeneza na kupitisha sheria na bajeti (mapato na matumizi ya fedha)

Bunge linalokuwa na wawakilishi waliochaguliwa na wananchi (Norwe linaitwa Stortinget maana yake ni Bunge)

Mamlaka ya kiutendaji

Linahakikisha kwamba kile ambacho bunge au mamlaka ya kutunga sheria imeamua inatekelezwa.

Serikali

Mamlaka ya kuamua kwa kutumia sheria ya hukumu

Inatafisiri sheria na kuhukumu kutokana na sheria

Mahakama

Mgawanyo wa uongozi (madaraka) kati ya watu au taasisi mbalimbali mara nyingi hutumika katika maeneo mengi zaidi ya mgawanyo huu wa serikali wenye sehemu tatu. Nchini Norwe, kwa mfano, tumekabidhi baadhi ya uongozi (mamlaka) ya ndani kwa uongozi kwa serikali za mitaa katika manispaa na mabaraza ya mikoa. Kinyume cha mgawanyiko huu wa uongozi kwa mamlaka itakuwa utawala wa mabavu (udikteta), ambapo nguvu zote ziko kwa mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu wanao ongoza nchi.

Kuzuia rushwa na mgongano wa maslahi

Ikiwa mtu anapata nguvu nyingi ya uongozi katika mamlaka ya kisiasa kwa sababu ana pesa nyingi au kwa sababu ni rafiki wa karibu au ni familia na mtu katika serikali, hii inaweza kuwa tatizo kwa demokrasia. Hebu fikiria mfanyabiashara tajiri akiwapa wanasiasa pesa za kupigia kura suala ambalo kampuni yake inataka kupata pesa. Hii inaitwa rushwa na ni kinyume cha sheria. Demokrasia inayofanya kazi vizuri ni ile yenye rushwa (ufisadi) kidogo.

Mwanasiasa akifanya maamuzi ili kujinufaisha yeye mwenyewe, rafiki wa karibu, ndugu au watu wa karibu na familia yake, mwanasiasa huyo anakuwa ameingia katika mgongano wa maslahi hivyo anakuwa amefanya jambo la kupendelea upande mmoja kwa kuangalia maslahi au faida yake zaidi. Kwa mfano, kukiwa na kesi kwa Waziri wa Viwanda na Biashara halafu rafiki wa karibu au ndugu wa waziri anahusika, waziri lazima ajitangaze kuwa hafai kuamua juu ya hiyo kesi. Hii ina maanisha anasema hawezi kushughulikia kesi hiyo kutokana na uhusiano wake na mtu ambaye kwa namna fulani anahusika katika kesi hiyo. Ikiwa mtu katika serikali hatasema katika kesi kama hiyo, atakuwa amekiuka sheria za mtu kushiriki katika maamuzi bila ya kuwa na upendeleo, mara nyingi hupelekea mtu huyo kuondoka serikalini. Wakati mwingine ikiwa ni hali mbaya, anaweza kupewa adhabu.

Sheria dhidi ya ufisadi au rushwa na uvunjaji wa upendeleo, zinalenga kumzuia mtu kupata mamlaka au uongozi kwa nguvu kwa sababu tu ana pesa nyingi au kwa sababu anamjua mtu mwenye madaraka.

Kuhusu yaliyomo kwenye filamu hapo chini

Hii filamu au video fupi iliyopo hapa chini inazungumzia maswali kuhusu kutokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi na uaminifu kwa wanasiasa. Filamu iko kwa Kinorwe, na hapa kunakuja maelezo kuhusu yaliyomo.

Fikiria kuwa wanataka kujenga barabara ya magari pale unapoishi. Barabara hii itapita moja kwa moja ndani ya shamba dogo (bustani) ya mdogo wake meya. Ghafla meya anabadilisha mawazo na kusema hapana juu ya ujenzi wa barabara hiyo. Anasema kwamba ni kwa sababu ujenzi wa barabara hiyo ni mbaya kwa mazingira. Sasa inakuwa vigumu kujua kama meya anasema hapana ili kulinda mazingira, au ni kwa sababu anataka kulinda shamba dogo (bustani) la ndugu yake. Kwa sababu ya tatizo hilo, meya hana uwezo wa kushughulikia suala hili na hawezi kuliamua. Hivyo, manispaa inapaswa kumtafuta mtu mwingine wa kuchukua nafasi ya meya katika suala kufanyia kazi ujenzi barabara. Wanasiasa wanapaswa kuhakikisha kwamba watu wanaweza kuwa na imani wanapoamua kuhusu jambo fulani, ni kwa sababu kile wanachoamua ndiyo huwa jambo bora kwa jamii.

 

Ulinzi wa maslahi ya watu binafsi na walio wachache

Katika nchi ya kidemokrasia watu wengi ndio wanaofanya maamuzi. Lakini je, itakuwaje kama watu walio wengi, wakiamua kuwatesa baadhi ya watu walio wachache au makundi ya watu yaliyo maalumu katika jamii? Labda watu wengine wakanyang’anywa nyumba zao, haki ya kupiga kura, uhuru wa kuongea, au uraia wao. Labda wengine wakaishia kufungwa gerezani au wananyongwa bila ya kufunguliwa kesi. Makundi yote katika jamii yanaweza kuzuiwa kutekeleza dini zao au utamaduni wao. Makundi ya watu walio wachache yanaweza hata kujaribiwa kuteketezwa kabisa. Mambo haya yote yanatokea leo katika nchi nyingi zinazodai kuwa za kidemokrasia. Ndiyo maana watu walio wachache na makundi ya watu walio wachache wanahitaji haki zitazowalinda dhidi ya unyanyasaji au ukandamizwaji na ubaguzi.

Sort-hvitt foto av en mann som står i en åpen bil. Det er tett i tett med folk rundt bilen.
Ingawa Adolf Hitler alianzisha utawala wa kutumia nguvu kwa haraka nchini Ujerumani, mwanzoni alichaguliwa kidemokrasia. Mara tu baada ya ushindi wake wa uchaguzi mwaka 1933, mateso kwa Wayahudi na makundi ya watu walio wachache yalianza nchini Ujerumani. Ujerumani mwanzoni mwa mwaka 1933 ni mfano wa jinsi uamuzi unaofanywa na watu wengi unaweza kusababisha unyanyasaji wa kikatili dhidi ya wachache na watu binafsi.

Utawala wa kisheria

Utawala wa kisheria ni kanuni muhimu katika demokrasia na inapaswa kumlinda mtu dhidi ya kuhukumiwa bila ya kujulikana kama ni kweli alifanya makosa (hatia). Hapa kuna baadhi ya kanuni ambazo zinapaswa kuwepo ili kuwa na utawala wa kisheria:

  • Maamuzi yote ya mamlaka za serikali inayofanya yanatakiwa kufuata sheria za nchi
  • Mtu hawezi kuhukumiwa bila kufunguliwa kesi.
  • Mtu ana haki kesi yake kusikilizwa katika mahakama isiyoegemea upande wowote.
  • Mtu huchukuliwa kuwa hajafanya kosa (hatia) hadi kuwe na ushahidi.
  • Kila mtu yupo sawa mbele ya sheria; hakupaswi kuwa na ubaguzi usio wa haki.
  • Kila upande katika kesi unapaswa kupewa nafasi ya kutoa maelezo yake kuhusu kesi.

Haki zinazolinda jamii ya watu walio wachache

Katika haki za binadamu za Umoja wa Mataifa, ulinzi wa makundi ya jamii ya watu walio wachache na makundi ya watu yaliyo hatarini ni jambo la msingi. Watu wanaoishi maisha yao kiasili wana ulinzi maalumu. Watu wanaoishi kiasili ni makundi ya watu walio tofauti na watu wengi katika nchi, na ambao wamekuwepo katika nchi muda mrefu, kabla ya mipaka ya nchi na serikali kuanzishwa. Watu wanaoishi kiasili kwa kawaida wamekabiliwa na ubaguzi na unyanyasaji kutoka kwa serikali (mamlaka) na kutoka kwa watu wengi. Haki za watu wanaoishi kiasili zinatakiwa kuhakikisha kwamba ubaguzi na unyanyasaji kama huo hautokei, na kusaidia watu wanaoishi kiasili kutunza utamaduni na lugha zao.

Nchini Norwe, kuna watu wanaoishi kiasili, wanaitwa Same. Lakini pia tuna makundi matano ya watu walio wachache wa kitaifa wanaitwa ” Kvens/norskfinner, skogfinner, Wayahudi, romer na watu wa roma (romanifolk)/tatere. Haya ni makabila yenye utamaduni wao, ambao wana uhusiano wa muda mrefu na nchi. Watu walio wachache katika taifa, wana baadhi ya haki sawa na watu wanaoishi kiasili, lakini watu wanaoishi kiasili wana ulinzi mkubwa katika baadhi ya maeneo.

Katika nchi ya kidemokrasia, hakuna mtu anayepaswa kubaguliwa au kuteswa kwa sababu yoyote ile. Nchini Norwe, tuna sheria zetu zinazotulinda dhidi ya ubaguzi kwa misingi ya mfano wa dini, kabila, jinsia, na nani unapenda kuwa nae kimapenzi (kujamiiana), utambulisho wako kijinsia (kama wewe ni mwanaume,mwanamke au uko na ulemavu).

Haki zinazolinda watu walio wachache ni muhimu zinatukumbusha juu ya msingi wa demokrasia, yaani kwamba watu wote wanazaliwa huru na wakiwa na utu, thamani sawa na haki za binadamu.

Arbeidsoppgaven inneholder sentrale ord i den norske teksten. // Kazi hii ina maneno muhimu katika maandishi ya Kinorwe.

  • Oversett ordene ved hjelp av LEXIN eller på annen måte.// Tafsiri maneno kwa kutumia LEXIN au njia nyingine.
  • I høyre kolonne er ordet brukt i en setning som finnes i teksten. Oversett eller forklar hva setningen betyr. // Katika safu wima ya kulia, neno hilo limetumika katika sentensi inayopatikana katika maandishi. Tafsiri au eleza maana ya sentensi hiyo.

Viktige ord i “Hva er demokrati?”

Viktige ord i “Hva er demokrati?“// Maneno muhimu “Demokrasia ni nini?”