Hva er FN?// Umoja wa Mataifa ni nini?
FN ni jina la Kinorwe la shirika la Umoja wa mataifa ( kingereza UN). UN ni kifupi cha Umoja wa Mataifa kwa lugha ya kingereza, na FN ni kifupi cha Umoja wa Mataifa kwa lugha ya kinorwei. Umoja wa Mataifa unafanya kazi kwa ajili ya amani, haki na ushirikiano kati ya nchi mbalimbali duniani. Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwaka 1945, mara tu baada ya Vita kuu ya pili ya dunia. Lengo lilikuwa ni kuzuia vita kubwa zaidi.
Karibia kila nchi duniani ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Wamekubaliana kufanya kazi pamoja kutatua matatizo kama vile vita, umaskini, magonjwa na mabadiliko ya tabia nchi. Makubaliano hayo yanaitwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Nembo ya Umoja wa Mataifa ina maduara matano na ramani ya dunia yenye rangi nyeupe. Karibu na ramani kuna matawi mawili ya mti wa mizeituni. Matawi ya mti wa mizeituni inaashiria kuwa Umoja wa Mataifa unalenga kulinda amani na kutengeneza usalama katika dunia.
Siku ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa huadhimishwa kila mwaka tarehe 24 Oktoba.

UN au Umoja wa mataifa unafanya nini?
Umoja wa mataifa unakazi nyingi muhimu. Chini unaweza kusoma kuhusu baadhi ya kazi zao.
Amani na usalama
Umoja wa mataifa unafanya kazi kuwa na dunia iliyo salama. Wakati mwingine migogoro hutokea kati ya nchi na nchi. Umoja wa Mataifa unaweza kusaidia kupatikana suluhu kwa njia ya amani. Kama vita ikitokea, Umoja wa Mataifa unaweza kutuma wanajeshi ili kulinda watu. Wanaweza pia kusaidia kujenga upya jamii baada ya vita.
Msaada wa dharura
Umoja wa Mataifa husaidia watu wanaoishi katika maeneo ya vita, majanga ya asili au umasikini. Wanaweza kutoa chakula, maji, dawa na mahali pa kulala. Wakati mwingine Umoja wa Mataifa huwasaidia watu wanaolazimika kukimbia.
Haki za binadamu
Umoja wa Mataifa unafanya kazi ili kuhakikisha kwamba watu wote duniani wanatendewa haki na kwa heshima. Umoja wa Mataifa umetoa orodha inayosema watu wote wana haki zipi. Orodha hiyo inaitwa Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu. Haki za binadamu zinahusu haki ya kuishi kwa usalama, kwenda shule, kutoa maoni yako na kuhudumiwa au kutendewa kwa usawa bila kujali wewe ni nani. Nchi zote katika Umoja wa Mataifa lazima zifuate haki za binadamu.
Mkataba wa Haki za Mtoto
Watoto wanahitaji ulinzi wa ziada na kwa hiyo wana haki zaidi. Haki hizi zinaitwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto. Inahusu watoto wote kuwa na haki ya kutunzwa, kuwa salama na kuwa na maisha mazuri. Umoja wa Mataifa unahakikisha kwamba nchi zote zinafuata sheria katika mkataba huo, ili watoto wawe na maisha mazuri bila kujali wanaishi wapi.
Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa
Malengo ya Maendeleo Endelevu ni orodha ya malengo 17 ambayo yataifanya dunia kuwa mahali pazuri zaidi kwa watu na vitu vya asili. Malengo yanahusu kumaliza umaskini na kuhakikisha kuwa kila mtu anaenda shule. Pia zinahusu kukomesha ongezeko la joto duniani na kutunza wanyama, mimea na dunia.
Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa

Kazi muhimu ya mkutano mkuu ni kujadili jinsi ya kutatua changamoto kubwa zaidi za ulimwengu. Mkutano mkuu unaundwa na wawakilishi kutoka nchi zote ambazo ni wanachama. Kila nchi ina fursa ya kutoa maoni yake na kupiga kura juu ya suluhisho zinazopendekezwa. Mkutano Mkuu hukutana kipindi cha msimu wa vuli (ambacho huwa kuanzia mwezi wa tisa hadi mwezi wa kumi na moja) katika jengo la umoja wa mataifa (UN). Jengo la Umoja wa mataifa liko New York, Marekani.
Kwa nini Umoja wa mataifa (UN) ni muhimu?
Umoja wa Mataifa ni shirika muhimu kwa sababu karibu nchi zote duniani hufanya kazi pamoja ili kuifanya dunia kuwa mahali pazuri zaidi. Umoja wa Mataifa unafanya kazi ya kuleta amani, kukomesha vita, kusaidia watu masikini au waliokimbia makazi yao, na kulinda asili na mazingira yetu. Pia inahakikisha kwamba watu wote na hasa watoto wanapata haki zao na kutendewa haki.