Informasjon om norsk grunnskole // Taarifa kuhusu shule ya msingi Norwe
On behalf of the Parental Advisory Committee for Primary Education ( FUG ), NAFO has developed information about Norwegian primary school. The material is available in several languages in addition to Norwegian, and can be used to support home-school cooperation. The information is available in text and audio. It is also possible to download the content as a booklet in PDF format. NAFO has developed information about Norwegian primary school based on the work assigned to them by the Parental Advisory Committee for Primary Education ( FUG ). This information is available in several languages other than Norwegian, and can be used to support home-school cooperation. The information is available in text and audio. and can be downloaded as a PDF file.
Bonyeza kwenye kichwa cha habari na sikiliza sauti
Shule ya msingi Norwe
Elimu ya shule ya msingi ni miaka kumi na imegawanywa katika shule ya msingi (barneskole) na shule ya sekondari (ungdomsskole). Kuna madarasa saba katika elimu ya shule ya msingi (barneskole). Elimu ya shule ya sekondari (ungdomsskole) ina madarasa matatu. Watoto wanaanza shule mwaka ule wanaotimiza miaka sita, na wanaenda kusoma darasa linalofuata kila baada ya msimu wa jua na joto (kiangazi).
Mwaka wa masomo unaanza katikati ya mwezi wa nane hadi karibu na tarehe 20 mwezi wa sita. Katika ratiba ya mwaka ya shule (skoleruta) utaona siku gani kuna likizo na siku ambazo hakuna shule katika mwaka wa masomo wa shule. Unaweza kupata ratiba ya mwaka wa masomo ya shule (skoleruta) shuleni. Pia unaweza ipata kwenye intaneti (tovuti website) ya halmashauri (kommune).
Shule za msingi za umma ni bure
Kuna shule za msingi za umma na binafsi. Halmashauri (kommune) ndio yenye shule za msingi za umma. Haulipii kusoma katika shule za umma. Inamaanisha kufundishwa, vifaa na shughuli zote zinazofanyika katika kujifunza ni bure. Watoto wote wenye umri unaotakiwa kwenda shule wana haki ya kwenda katika shule za umma. Miaka ya lazima mtu kwenda shule ni miaka 6 hadi 16.
Kutokuwepo na ruhusa
Nchini Norwe ni lazima watoto wote wenye miaka ya kwenda shule kwenda shule. Hii ina maana kwamba mwanafunzi anatakiwa kuwepo shuleni siku zote za masomo na kuwepo wakati wanafundishwa kila siku za shule. Kwa hiyo, wazazi hawawezi kuamua wenyewe kama mwanafunzi atakaa nyumbani bila kwenda shule. Shule huandika na kufuatilia kama mwanafunzi yupo shuleni kila siku. Ikiwa mwanafunzi ni mgonjwa kiasi kwamba hawezi kwenda shule, wazazi wanaweza kumuacha abaki nyumbani. Wazazi wana jukumu la kuijulisha shule wakati mwanafunzi ni mgonjwa. Shule inapaswa kupewa taarifa asubuhi kabla masomo kuanza. Ikiwa mwanafunzi ataumwa kwa siku nyingi, inapaswa kupata cheti cha ugonjwa (sykemelding) kutoka kwa daktari.
Ikiwa ni lazima mwanafunzi apate ruhusa ya kutokuwepo shuleni tofauti na muda wa likizo na siku za mapumziko zilizotajwa katika ratiba ya mwaka wa masomo shuleni (Skoleruta), wazazi wanapaswa kuomba ruhusa hiyo mapema. Katika maombi hayo, lazima waeleze kwa nini ni muhimu mwanafunzi apewe ruhusa ya kutokuwepo. Manispaa (kommune) inaweza kutoa ruhusa ya kutokuwepo kwa muda wa hadi majuma mawili, ikiwa itaona kwamba kufanya hivyo kuna sababu za msingi. Wanafunzi ambao ni wanachama wa jumuiya ya kidini ambayo si Kanisa la Norwe (Den norske kirke) wana haki ya kupata ruhusa ya kutokuwepo shuleni katika siku ambazo jumuiya yao ya kidini ina sikukuu. Hata hivyo, ni lazima waombe ruhusa kwa siku hizo.
Maadili muhimu katika shule Norwe
Maadili katika shule za Norwe yamejengwa katika misingi ya haki za binadamu. Thamani ya binadamu na hali ya kuwa salama ni maadili muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa katika kila jambo linalofanyika shuleni.

Wanafunzi wote wanatakiwa kuwa salama na vizuri shuleni
Shule inatakiwa kumpokea mwanafunzi kwa heshima na uaminifu. Hakuna mwanafunzi anaetakiwa kutengwa ama kusumbuliwa kwa njia yoyote ile. Wanafunzi wote wanatakiwa kujisikia kuwa sehemu ya darasa na shule. Wafanyakazi wote wa shule wanatakiwa kufuatilia kuwa wanafunzi wapo vizuri shuleni. Ikiwa mtu mzima anayefanya kazi shuleni anajua, anahisi au ana amini kwamba mwanafunzi anafanyiwa unyanyasaji, uonevu, kusumbuliwa, au kwa njia nyingine yoyote hajisikii vizuri shuleni, anapaswa:
- Kuingilia na kuzuia kitendo cha unyanyasaji mara moja, kama inawezekana.
- Kutoa taarifa kwa mkuu wa shule (rektor)
- Kuchunguza kile kilichotokea
Ikiwa mwanafunzi anahisi kwamba hayuko salama na vizuri shuleni, mkuu wa shule anatakiwa kutengeneza mpango na kuchukua hatua ili mwanafunzi ajisikie kuwa salama na vizuri shuleni tena. Hii ni jukumu la shule la kuchukua hatua haraka kama mwanafunzi hajisikiii vizuri (aktivitetsplikt).
Kanuni na tabia
Shule zina sheria au utaratibu kwa ajili ya kanuni na tabia ambazo mwanafunzi anatakiwa kuzifuata. Katika shule za Norwe, mambo yanayohusu kanuni na tabia hushughulikiwa kupitia mazungumzo. Ikiwa shule inaona kwamba mwanafunzi hafuati kanuni hizo, hatua ya kwanza ni kuzungumza na mwanafunzi kuhusu jambo hilo. Ikiwa mwanafunzi ataendelea kuvunja kanuni baada ya mazungumzo hayo, shule itawasiliana na wazazi ili wajue kilichotokea na waweze kuzungumza na mtoto wao nyumbani kuhusu suala/jambo hilo. Mbali na kanuni za shule, kila darasa linaweza kuwa na kanuni zake (trivselsregler) ambazo wanafunzi na mwalimu hutengeneza kwa pamoja. Kanuni hizo zinaeleza jinsi wanavyotaka mazingira ya darasani yawe ili kila mtu ajisikie vizuri na aweze kujifunza vizuri zaidi.
Wanafunzi wote wanatakiwa kuwa na nafasi sawa ya kujifunza.
Shule inatakiwa kuwapa nafasi sawa wanafunzi wote kwa ajili ya kujifunza na kujiendeleza bila ya kujali walipotoka na uwezo walionao. Shule inatakiwa kuzingatia kuwa wanafunzi wapo tofauti na inatakiwa kuchangia mwanafunzi ajisikie kuwa yupo nyumbani akiwa shuleni na katika jamii. Ufundishaji unatakiwa kumpa mwanafunzi ujuzi na hamu ya kujifunza katika maisha yake yote. Shule inatakiwa kuchangia:
- mwanafunzi kujiendeleze yeye kama binadamu
- kukuza uwezo wake katika masomo
- kujisikia kuwa ni sehemu ya jamii

Ufundishaji unaoangalia uhitaji wa mwanafunzi
Wanafunzi wote wanatakiwa kupata ufundishaji unaoangalia uhitaji wa mwanafunzi (tilpasset opplæring). Wanafunzi wapo tofauti na wanajifunza kwa njia tofauti. Shule inatakiwa kufundisha katika njia ambayo kila mwanafunzi anaweza kupata kuelewa vizuri kile kinachofundishwa.
Ufundishaji unaopangwa kulingana na uhitaji wa mwanafunzi
Baadhi ya wanafunzi wana haki ya kupata ufundishaji unaopangwa kulingana na uhitaji wao (Individuelt tilrettelagt undervisning). Iwapo wazazi au shule wanaona kwamba mwanafunzi hajifunzi vizuri na kwa kutosha, shule inapaswa kuweka mipango ya kumfundisha mwanafunzi, inayoendana na uhitaji yake. Ikiwa hatua hizo hazitoshi kuboresha maendeleo ya mwanafunzi, basi shule pamoja na huduma ya Kisaikolojia na ushauri wa Kielimu (Pedagogisk-psykologisk tjeneste PPT), kwa kushirikiana na mzazi, wataangalia kama mwanafunzi anahitaji hatua na msaada wa ziada ili apate elimu nzuri(bora). Hatua hizo za ziada huitwa ufundishaji uliopangwa kulingana na uhitaji wa mwanafunzi (kwa lugha ya kinorwe Individuelt tilrettelagt undervisning). Ufundishaji uliopangwa kulingana na uhitaji wa mwanafunzi (Individuelt tilrettelagt undervisning), kwa mfano unaweza kuwa kwamba mwanafunzi anajifunza kwa kufuata malengo tofauti ya kujifunza/kusoma na wanafunzi wengine au mwanafunzi anatumia vifaa maalumu, na kwamba mwanafunzi anaweza kupokea usaidizi wa ziada kutoka kwa mtu mzima shuleni (wakati wa kufundishwa na wakati wa mapumziko).
Ushirikiano kati ya nyumbani na shule
Sheria ya mafunzo inasema shule na wazazi wapo na jukumu la pamoja katika mafunzo ya elimu ya msingi. Shule inawajibu wakushirikiana na wazazi. Ushirikiano unakuwa kwa ngazi ya taifa na katika shule moja.

Ushirikiano katika ngazi ya kitaifa
Uongozi wa Norwe umeweka kamati ya kitaifa ya Wazazi kwa shule za msingi na Sekondari ya Juu (kwa kinorwe inaitwa foreldreutvalg for grunnskolen og den videregående skolen FUG). Kamati ya kitaifa ya Wazazi kwa shule za msingi na Sekondari ya Juu hutoa ushauri na mwongozo kwa wazazi pamoja na shule. Pia hutoa ushauri kwa uongozi kuhusu masuala yanayohusu ushirikiano kati ya nyumbani na shule.
Ushirikiano na shule
Wazazi wa wanafunzi shuleni hushiriki katika kuchagua Kamati ya Wazazi ya Shule (kwa lugha kinorwe foreldrenes arbeidsutvalg FAU). Kamati ya Wazazi ya Shule (kwa lugha ya kinorwe foreldrenes arbeidsutvalg FAU) hushirikiana na shule na kutoa ushauri kwa mkuu wa shule. Katika shule nyingi, pia huchaguliwa mwakilishi wa wazazi wa darasa (kwa lugha ya kinorwe klassekontakt). Mwakilishi huyu huchaguliwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wa shule na hushirikiana na walimu wa darasa. Mwakilishi wa wazazi huwasilisha mawazo au mapendekezo (maoni) kwa niaba ya wazazi wote shuleni.
Ushirikiano darasani
Kila shule inapaswa kuandaa mkutano wa wazazi mwanzoni mwa mwaka wa masomo wa shule. Shule nyingi huwa na mikutano miwili ya wazazi katika kipindi cha mwaka wa masomo wa shule, na baadhi huwa na mikutano zaidi. Mikutano ya wazazi huwahusisha wazazi wote wa wanafunzi katika darasa moja au kwa madarasa yote kwa ujumla. Katika mikutano hiyo, wazazi hupewa taarifa kuhusu shule, mwaka wa masomo wa shule na mipango na taratibu zinazofuatwa shuleni. Pia hupewa maelezo kuhusu wanachofundishwa watoto kwenye masomo na mambo mengine muhimu ambayo mzazi anapaswa kuyafahamu. Mikutano ya wazazi pia huwapa wazazi nafasi ya kufahamiana. Wazazi wanapofahamiana, huwa rahisi kushirikiana kuhusu watoto wao, jambo ambalo ni muhimu watoto wanapokuwa pamoja shuleni na hata wakati wapo katika michezo wakiwa nje ya shule.
Ushirikiano kuhusu mtoto wako
Wazazi wana nafasi muhimu katika mafanikio ya mtoto wao shuleni. Ni muhimu shule na wazazi washirikiane vizuri ili kumsaidia mwanafunzi kufanikiwa katika masomo yake. Kama mzazi, unapaswa kuhudhuria mkutano wa maendeleo ya mwanafunzi na mikutano ya wazazi. Pia ni muhimu kuonyesha kuwa unajali na kufuatilia maendeleo ya mtoto wako shuleni. Ili shule iweze kumsaidia mtoto wako kwa njia bora zaidi, ni muhimu uwape walimu taarifa muhimu kuhusu mtoto wako ambazo zinaweza kusaidia katika elimu na ustawi wake. Je unawezaje kuonesha kuwa unajali masomo/shule ya mtoto wako?
Kuna vitu vingi wewe kama mama au baba unaweza kufanya kuweza kuonesha kuwa unajali masomo/shule kwa mtoto wako. Unaweza
- kuzungumza na mtoto/kijana wako kuhusu alichofanya na alichojifunza shuleni
- kutenga muda ili mtoto/kijana wako aweze kufanya kazi za kufanya nyumbani kutoka shuleni (hjemmelekse)
- kuwa karibu na kumsaidia mtoto wako anapofanya kazi za kufanya nyumbani kutoka shuleni (hjemmeleske)
- shiriki katika mikutano na vitu vingine vinavyopangwa shuleni
- wasiliana na shule ikiwa unahitaji kuuliza swali, kuzungumza kuhusu jambo fulani, kutoa au kupata taarifa muhimu.
Mkutano wa maendeleo
Mkutano wa maendeleo ni mkutano kati ya mwanafunzi, mzazi na mwalimu wa darasa. Katika mkutano mwanafunzi, mzazi na mwalimu watazungumza juu ya maendeleo ya mtoto shuleni. Malengo ya mazungumzo ni kuweza kujua ni jinsi gani shule na wazazi wanaweza kushirikiana kumsaidia katika masomo na masuala ya kijamii. Jambo lingine muhimu ni jinsi gani mwanafunzi yeye mwenyewe anaweza kujifunza vitu shuleni mwenyewe. Mwanafunzi na wazazi wanakutana na mwalimu wa darasa mara mbili katika mwaka mmoja wa masomo wa shule. Zungumza na mtoto wako kabla ya mkutano wa maendeleo. Fikiria Kama upo na maswali kwa ajili ya shule. Ukiacha mkutano, shule ina wajibu wakufanya mawasiliano na wewe kama mzazi kama kuna uhitaji. Mkutano wa wazazi unaweza kufanyika kati ya wazazi na mwalimu bila ya kuwa na mwanafunzi.
Wajibu wa kuweka siri
Wote wanaofanya kazi katika shule wana wajibu wa kuweka siri. Hii inamaanisha hawatakiwi kutoa taarifa kwa mtu mwingine kuhusu taarifa binafsi walizopata kujua kuhusu wewe ama mtoto wako kazini. Ni kosa kisheria kutoa taarifa zinazopaswa kuwekwa katika usiri.
Kuna sehemu mbili ambazo sheria inaweza isifuatwe:
- Kama mtoto wako anauhitaji wa msaada wa ziada ama usaidizi kutoka kwa watu wengine nje ya shule. Unaweza kutoa ruhusa kwa shule kuwapa taarifa muhimu wale watakao msaidia mtoto. Kuwapa ruhusa (samtykke) Ina maanisha unawapa ruhusa shule kuwaambia juu ya kitu fulani watu wengine. Wewe na shule mnatakiwa kukubaliana ni kitu gani wanaweza kusema. Ruhusa Kama hiyo inakuwa na mipaka ya muda na unaweza kukata kuendelea nayo muda wowote.
- Ikiwa shule ina sababu ya kuamini kwamba mtoto hapatiwi malezi vizuri au yuko katika hatari ya kuumizwa kwa njia yoyote, wafanyakazi wa shule wana wajibu wa kuripoti kwa huduma za ustawi wa watoto (barnevernet).
Mtafsiri
Ni muhimu shule na wazazi wawasiliane vizuri na kuelewana. Wakati mwingine kuna weza kuwa na haja ya kutumia mtafsiri. Shule na wewe mzazi, mnaweza kuomba kutumike mtafsiri. Ukihitaji mtafsiri katika mkutano wa wazazi, lazima uiambie shule mapema. Shule ina jukumu la kuweka nafasi na kumlipa mtafsiri. Mtafsiri ana wajibu wa kuweka usiri. Hairuhusiwi kuwatumia watoto kama watafsiri.
Mtaala wa elimu
Sheria ya mafunzo (elimu) inasimamia elimu katika shule za msingi na sekondari ya juu, na mtaala wa mafunzo unasimamia yale yatakayofundishwa katika kutoa elimu. Mtaala wa elimu (kwa lugha ya kinowe læreplanverket) una sehemu kuu (kwa lugha ya kinoweoverordnet) na mitaala (miongozo) tofauti kwa masomo.
Sehemu kuu ya mtaala wa elimu
Sehemu kuu ya mtaala inaeleza maadili na kanuni zinazopaswa kuongoza mafunzo. Inahusu mafunzo yote katika shule ya msingi na ya sekondari ya juu.
Sehemu hii kuu ya mtaala inaweka msisitizo kwamba wanafunzi wanapaswa kupata nafasi ya kukuza uelewa wa mazingira, uwezo wa kufikiri kwa kina na ufahamu wa kimaadili. Wanafunzi pia wanapaswa kujifunza maana ya demokrasia kwa vitendo.
Wanafunzi wanapaswa kukuza maarifa na uelewa wa vitu wa kudumu hatua kwa hatua. Wanapaswa kutafakari juu ya ujifunzaji wao wenyewe na kuweza kutumia kile walichojifunza katika mazingira tofauti. Wanafunzi wanapaswa kufanya mazoezi ya kutengeneza maswali na kutafuta majibu – wakiwa peke yao na pamoja na wengine. Wanafunzi wanapaswa kujifunza jinsi gani wanaweza kujifunza. Ushirikiano, fikra mpya na ubunifu, uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kutafakari, udadisi na uchunguzi ni mambo muhimu.
Mpango wa kujifunza masomo
Mpango wa kujifunza masomo unaeleza nini kile wanafunzi watasoma katika madarasa tofauti. Baadhi ya shule wana amau wao jinsi gani wanafunzi watafikia malengo ya mpango wa kujifunza masomo.
Kupima (Tathmini)
Kuanzia mwaka wa kwanza wa masomo, wanafunzi wanapaswa kupokea taarifa ya kupima (tathmini) yenye kuendelea kutoka kwa walimu wao. Taarifa ya kupima (tathmini) ni za maana sana ili mwalimu ajue namna ya kumsaidia kila mwanafunzi kulingana na uwezo wake. Pia, taarifa ya kupima (tathmini) zinamsaidia mwanafunzi kuelewa mambo ambayo anaweza kufanya yeye mwenyewe ili aweze jifunze vizuri zaidi. Taarifa ya kupima (tathmini) kuhusu masomo, tabia au nidhamu na mwenendo hutolewa mwaka mzima. Mwalimu anaweza kutoa taarifa ya kupima (tathmini) kwa njia ya kusema (mdomo) au kwa kuandika. Katika madarasa ya shule ya msingi, wanafunzi hawapewi alama au maksi (karakter). Lakini katika madarasa ya shule za sekondari ya chini (Ungdomsskolen), wanafunzi wanapata taarifa ya kupima (tathmini) zenye alama na pia zisizo na alama. Alama zinatoka 1 mpaka 6, na alama ya 6 ndiyo ya juu zaidi. Kila mwanafunzi pia anatakiwa kujitathmini, maana yake aangalie kazi yake mwenyewe, maendeleo yake, na uwezo wake ili ajue anafanya vizuri wapi na anahitaji kuboresha wapi. Hii ndiyo inaitwa kujipima (kujitathmini) mwenyewe (kwa lugha ya kinorwe egenvurdering).
Mwanafunzi ambae ana lugha ya mama nyingine zaidi ya kinorwe
Mwanafunzi ambae ana lugha ya mama (lugha ya kwanza) nyingine zaidi ya kinorwe au sami, ana haki ya kupata masomo maalumu ya lugha mpaka atakapojifunza Kinorwe vizuri, kiasi cha kuweza kufuata masomo ya kawaida pamoja na wanafunzi wengine darasani. Masomo haya maalumu ya lugha yanaweza kuwa ya aina tatu.
- Masomo ya ziada ya lugha ya kinorwe (Forsterket norskopplæring). Ina amanisha mwanafunzi anapatiwa muda wake wa kujifunza zaidi lugha ya kinorwe.
- Mafunzo kwa lugha mbili katika masomo – Mwanafunzi anasaidiwa kuelewa masomo kwa kutumia lugha yake ya mama pamoja na kinorwe.
- Mafunzo kwa lugha ya mama – Kufundishwa na kujifunza lugha yake ya mama (lugha ya kwanza).
Shule inatakiwa kumpima mwanafunzi ujuzi wake wa lugha ya kinorwe ili kuweza kujua kama yupo na haki ya masomo ya ziada ya lugha ya kinorwe. Ikiwa matokeo ya kipimo yanaonyesha kwamba mwanafunzi ana haki ya kupata masomo hayo, shule itatoa uamuzi rasmi unaoeleza aina ya masomo atakayopata na muda au kiwango cha masomo hayo. Kama mzazi au mlezi, una haki ya kupinga (kukata rufaa) uamuzi huo ikiwa haukubaliani nao.
Masomo ya ziada ya lugha ya kinorwe
Mwanafunzi ambae hajakaa muda mrefu Norwe na hajajua vizuri lugha ya kinorwe, anaweza kupata masaa yake mwenyewe ya kujifunza lugha ya kinorwe zaidi. Baada ya muda atakapokuwa amejifunza na kujua zaidi lugha ya kinorwe, anaweza kuendelea kufuatilia masomo ya darasani huku akipata usaidizi wa ziada. Malengo ya masomo ya ziada ya kinorwe ni kumuwezesha mwanafunzi kujifunza lugha ya kinorwe kwa kutosha na kumuwezesha aweze kufuatilia masomo ya darasani bila ya usaidizi wa ziada. Inaweza kuchukua muda mrefu na mara nyingi miaka mingi kujifunza lugha ya kinorwe itakayokuwezesha kuweza kupata kuelewa kila kitu kwenye masomo yote yanayofundishwa kwa lugha ya kinorwe.
Mafunzo kwa lugha mbili katika masomo
Wakati mwanafunzi anaendelea kujifunza lugha ya kinorwe, pia anaendelea kusoma masomo mengine. Kwa sababu hiyo, inaweza kuwa lazima apewe msaada kwa kutumia lugha yake ya mama (lugha ya kwanza) ili aweze kuelewa masomo vizuri. Mwalimu wa somo na mwalimu anayefundisha kwa lugha mbili hufanya kazi pamoja kupanga mambo ambayo mwanafunzi atafundishwa kwa lugha yake ya mama. Hii inaitwa mafunzo kwa lugha mbili katika masomo (kwa kinorwe tospråklig opplæring i fag), maana yake mwanafunzi anafundishwa masomo kwa kutumia lugha mbili. Kama msaada huo unahitajika, mwanafunzi ana haki ya kupata elimu ya lugha mbili katika masomo.
Mafunzo kwa lugha ya mama
Masomo kwa lugha ya mama ni kufundishwa kwa kutumia lugha ya kwanza ya mwanafunzi. Lengo ni kumsaidia mwanafunzi ajifunze zaidi kwa kutumia lugha yake ya mama. Hii inaweza kumrahisishia mwanafunzi kujifunza lugha ya kinorwe. Shule inapaswa kupima (kutathmini) kama mwanafunzi anahitaji masomo ya lugha ya mama. Ikiwa shule itaona kwamba mwanafunzi ana yahitaji, basi mwanafunzi ana haki ya kupata masomo hayo.
Mpango wa kusaidia wanafunzi wapya
Wanafunzi ambao wamekaa muda mfupi tu nchini Norwe wanaweza kupewa nafasi ya kusoma katika darasa maalumu la kuanzia masomo (mwanzo), ili wajifunze lugha kabla hawajaanza kusoma kwenye madarasa ya kawaida. Manispaa (kommune) inaweza kupanga masomo haya katika vikundi maalumu, madarasa maalumu au hata shule maalumu kwa wanafunzi wapya waliofika nchini. Kujiunga na darasa maalumu la kuanzia (mwanzo) si lazima (hiari). Hata hivyo, wanafunzi wengi hufanya vizuri zaidi wanapoingia katika darasa la kawaida baada ya kuanza masomo kwenye darasa maalumu la kuanzia (mwanzo). Masomo yanayotolewa katika darasa maalumu la kuanzia (mwanzo) yanalenga kuwajumuisha wanafunzi na kuhakikisha mazingira mazuri ya kujifunzia.
Masomo nje ya darasa
Katika madarasa yote ni kawaida kwa wanafunzi kwenda kwenye matembezi, kutembelea makumbusho na kuwa na kitu cha kufanya (aktiviteter) nje ya darasa. Hii ni ufundishaji ulio sawa sawa na ufundishaji unaofanyika shuleni darasani, na ni lazima kushiriki.
Kwa shule nyingi ni kawaida wanafunzi kwenda kwenye kambi ya masomo (leirskole) kwa siku kadhaa na watoto wanalala huko. Malengo ya kambi ya masomo (leierskole) ni kuwajenga wanafunzi katika masomo na kijamii. Safari au matembezi ambayo shule inaandaa ni bure (hakuna kulipia). Kama unataka kujua kuhusu safari ya matembezi au kambi ya masomo (leierskole) unaweza kuwasiliana na mwalimu wa darasa kujua jinsi gani walivyopanga.
Kanuni ya kumpatia kila mwanafunzi elimu inayolingana na uwezo wake inatumika pia wakati wa masomo yanayofanyika nje ya darasa. Ni jambo la muhimu kwamba wanafunzi wote washiriki katika shughuli hizo. Ni muhimu wanafunzi wajifunze kwa njia mbalimbali, na safari au shughuli za nje ya darasa zinasaidia sana kuimarisha ushirikiano na urafiki kati ya wanafunzi wa darasa moja. Kama kuna jambo lolote linalofanya mtoto wako ashindwe kushiriki katika shughuli hizo, unapaswa kuzungumza na mwalimu wake wa darasa mapema ili shule iweze kufanya maandalizi yanayofaa na kumuwezesha mtoto wako kushiriki.
Kazi ya kufanya nyumbani
Ni kawaida wanafunzi kupewa kazi ya kufanya nyumbani baada ya muda wa shule. Kazi ya kufanya nyumbani inahusu vitu ambavyo wamejifunza shuleni, ambavyo mwanafunzi anatakiwa kujifunza zaidi nyumbani. Ni vizuri mzazi ukafuatilia na kuonesha kuwa unapenda na kujali kazi ya kufanya nyumbani aliopewa mtoto wako.
Kila shule huwa na usaidizi wa kufanya kazi za nyumbani. Usaidizi huo hotofautiana kati ya shule na shule na darasa lipi linalopewa usaidizi. Katika halmshauri (kommune) taasisi za kujitolea huwa zinatoa msaada kwa watoto katika kufanya kazi za kufanya nyumbani walizopata. Unaweza kuuliza shule kuna msaada gani unapatikana.
Muda wa mapumziko wa mwanafunzi
Watoto na vijana wanajifunza wakati wapo shule lakini pia muda wa mapumziko.
Programu ya shule ya muda wa mapumziko
Shule zote zina programu (huduma) za shule za kuwaangalia watoto muda wa mapumziko (kwa kinorwe skolefritidsordning SFO) kwa wanafunzi wa darasa la 1 hadi 4. Programu (huduma) ya kuwaangalia watoto muda wa mapumziko (kwa kinorwe skolefritidsordning SFO) ni huduma ya kuwaangalia, kuwajali na kucheza kabla na baada ya shule. Programu (huduma) ya shule kuwaangalia watoto muda wa mapumziko si bure, lakini baadhi ya halmashauri (kommune) programu (huduma) hii ni bure (haulipi kitu).
Michezo ya muda wa mapumziko
Watoto na vijana wengi wanashiriki katika michezo wakati wa muda wa mapumziko iliyopangwa, na hii inaweza kuwapa vitu vya kujifunza vingi. kama wanafunzi wanapenda vitu vinavyofanana vya kufanya wakati wa mapumziko inaweza kuwa rahisi kupata marafiki na kuchangia kuwa na mahusiano mazuri kati ya wanafunzi. Wazazi pia wanamchango mkubwa muhimu katika michezo ya watoto wakati wa mapumziko. Mara nyingi inakuwa wazazi wanashirikiana kuwapeleka na kuwarudisha watoto katika mazoezi na kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazoandaliwa. Wazazi wengi ni makocha (trener) au wanasaidia kwa njia nyingine pale watoto wao wanapokuwa katika michezo wakati wa muda mapumziko. Inaweza kuwa jambo zuri kwako kama mzazi kuzungumza na wazazi wengine ambao watoto wanacheza pamoja wakati wa muda wapumziko. Walimu wengi wanajua pia kuhusu vitu vingi kwenye michezo ya muda wa mapumziko ambayo wanafunzi wanacheza.
Kusherekea siku ya kuzaliwa
Ni kawaida kualika watu wakati wakusherekea siku ya kuzaliwa. Hii huwa zaidi wakati mtoto anakwenda shule ya msingi (barneskole). Watoto wengi wana aleji au aina ya chakula wanachopendelea ambapo inaweza kufanya kuwa shida kwao kushiriki katika sherehe. Ni jambo zuri kuwauliza wazazi wa watoto wengine kama watoto wao kuna kitu hawawezi kula kabla hawajaja katika shereya siku ya kuzaliwa. Ni kawaida kwenda na zawadi ndogo kwa ajili ya mtoto anaesherekea siku yake ya kuzaliwa. Inaweza kuwa jambo zuri kuzungumzia na kukubaliana zawadi ya siku ya kuzaliwa iwe kubwa kiasi gani wakati wa mkutano wa wazazi. Ni muhimu kufikiria kwamba hakuna mtu anayetengwa katika sherehe kama hizo.
Ushauri na kuendelea mbele na masomo
Haki ya msaada na ushauri kutoka kwa mshauri wa masomo
Shule inatakiwa kuchangia katika maendeleo binafsi ya mwanafunzi na maendeleo yake akiwa pamoja na wenzake (kijamii), lakini pia na maendeleo ya mwanafunzi kwenye masomo na katika kujifunza. Huduma ya kijamii na masomo (kwa lugha ya kinorwe sosialpedagogiske) inamsaidia mwanafunzi kuzoea na kujisikia vizuri shuleni. Huduma inapaswa kusaidia wanafunzi wenye matatizo ya peke yao (binafsi), ya kijamii, au ya kimawazo (kihisia) ambayo yanaweza kuathiri masomo yao na uhusiano wao na watu wengine (jamii) shuleni.
Msaada unaweza kuwa wa kuelewa tatizo ni nini, ukubwa wa tatizo na kujua nini shule inaweza kusaidia. Mwanafunzi anaweza kupata msaada nje ya shule pia. Msaada kutoka mshauri wa kijamii na masomo unaweza kuwa kutafuta na kufanya mawasiliano na sehemu inayoweza kutoa usaidizi.
Ushauri wa elimu (masomo) na kazi
Mshauri katika shule ya sekondari ya chini anampa mwanafunzi na wazazi taarifa kuhusu masomo ya sekondari ya juu (videregåenda) ambayo mwanafunzi anaweza kuomba nafasi.
Ushauri wa masomo (elimu) na kazi unalenga kusaidia wanafunzi kuwa na uelewa kuhusu maadili yao, vitu wanavyopenda, na uwezo wao. Hii inapaswa kumfanya mwanafunzi kujielewa na kuongeza uwezo wao wa kufanya uchaguzi mzuri wa masomo (elimu) na kazi. Washauri wanapaswa kusaidia wanafunzi kufikiria matokeo ya uchaguzi wanaofanya na wanapaswa kuzuia uchaguzi mbaya wa masomo (elimu) au kazi.
Mwanafunzi atapata taarifa na ushauri kuhusu
- Jinsi ya kuchagua kazi
- Masomo (elimu) yanayopatikana na anayoweza chagua Norwe na nchi nyingine
- soko la kazi kitaifa na kimataifa
- matumizi ya njia mbalimbali ya kupata ushauri
Kuingia shule ya sekondari ya juu (videregående)
Vijana waliomaliza elimu ya shule ya msingi, wana haki ya elimu ya sekondari ya juu (videregående). Wakati wanafunzi wanasoma darasa la 10 wanaomba nafasi ya masomo ya sekondari ya juu (videregående). Wanafunzi wanaokuja Norwe mwishoni mwa masomo ya sekondari, wanaweza kuwa na uhitaji wa masomo ya ziada ya shule ya msingi kabla ya kuanza masomo ya sekondari ya juu (videregåenda). Baadhi ya halmashauri (kommune) wana toa masomo ya mwaka mmoja wa ziada kwa elimu ya msingi. Sehemu nyingine wanafunzi wanaweza kwenda katika elimu ya watu wazima ama katika programu ya maandalizi kwa masomo ya sekondari ya juu. Sehemu nyingi kuna kile kinachoitwa darasa mchanganyiko ambapo vijana wanapata elimu ya msingi zaidi katika shule ya sekondari ya juu (videregående).


